Serikali yatoa vibali vya ajira mpya 86500 kwa mwaka wa 2024/25 na 2025/26 walimu, kada za afya, Sekta nyingine (Kilimo, Uhandisi n.k.).
Dodoma, Oktoba 11, 2025 — Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa jumla ya vibali vya ajira 86,500 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinakuwa na watumishi wa kutosha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, ametoa taarifa hiyo jijini Dodoma wakati akizungumza na vyombo vya habari, akibainisha kuwa ajira hizo zitagusa kada mbalimbali zikiwemo Elimu, Afya, Kilimo, Uhandisi na Sekta nyingine muhimu.
Utekelezaji wa Ajira za Mwaka 2024/25
Bw. Mkomi amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, Serikali ilitoa kibali cha ajira 45,000 kwa Taasisi mbalimbali.
- Mchakato wa utekelezaji ulianza tarehe 29 Aprili 2025, ambapo hadi sasa:
- Nafasi 30,863 zimejazwa na wahusika wamepangiwa vituo vya kazi.
- Nafasi 6,701 usaili umefanyika na wahusika wanatarajiwa kupangiwa vituo vya kazi ndani ya Oktoba 2025.
- Nafasi 7,436 zipo katika hatua ya mwisho ya ujazaji na zitakamilika Novemba 2025, kisha waombaji watapangiwa vituo vyao mara moja.
Ajira Mpya kwa Mwaka wa Fedha 2025/26
Kwa mwaka huu wa fedha 2025/26, Serikali imeidhinisha nafasi 41,500 za ajira mpya, zikiwemo:
| Sekta | Idadi ya Nafasi |
|---|---|
| Walimu | 12,176 |
| Kada za Afya | 10,280 |
| Sekta nyingine (Kilimo, Uhandisi n.k.) | 19,044 |
| Jumla | 41,500 |
Bw. Mkomi amesema utekelezaji wa vibali hivi unaanza mara moja, na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeelekezwa kuanza mchakato wa kujaza nafasi hizo sambamba na kukamilisha zilizobaki za mwaka 2024/25.
Maelekezo kwa Waajiri
Katibu Mkuu amewaagiza waajiri wote nchini kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira ili kuhakikisha lengo la ujazaji wa nafasi linatimia kwa wakati.
“Waajiri wanatakiwa kushirikiana kikamilifu na Sekretarieti ya Ajira. Aidha, wale waliokasimiwa madaraka ya kuendesha usaili kwa baadhi ya kada wahakikishe wanakamilisha mchakato huu mara moja kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma,” amesema Bw. Mkomi.
Ameelekeza pia kuwa usaili wa waombaji ufanyike kila Mkoa Tanzania Bara na katika vituo maalum vya Zanzibar ili kupunguza gharama na kuwapa nafasi waombaji kusailiwa katika maeneo yao.
Waombaji Watakaofaulu Usaili
Waombaji watakaofaulu usaili lakini wakakosa nafasi kwa sasa, wataingizwa kwenye kanzidata maalum na watapangiwa kazi kwa kadri nafasi mpya zitakapopatikana.
Aidha, barua za kupangiwa vituo kwa waombaji waliopangiwa kazi zitapatikana kupitia Mfumo wa Ajira (Recruitment Portal) kwenye akaunti za wahusika.
Dhamira ya Serikali
Bw. Mkomi amehitimisha kwa kusema kuwa Serikali itaendelea kutoa vibali vya ajira kulingana na mahitaji ya sekta mbalimbali ili kuhakikisha huduma bora zinafika kwa wananchi wote.
“Serikali imejipanga kuhakikisha kila sekta inakuwa na watumishi wa kutosha kwa ajili ya kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi kote nchini,” amesisitiza Katibu Mkuu Mkomi.
Chanzo: Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUU)
Tarehe: 11 Oktoba 2025, Dodoma
Soma zaidi:
Leave a Reply
View Comments